Muungano wa Afrika, AU, umetoa wito
kwa viongozi wa mataifa matano kuishawishi Burundi kukubali kikosi
maalum cha kudumisha amani kufuatia miezi kadhaa ya ghasia za kisiasa
nchini humo.
Kamati hiyo maalumu ya AU, inamshirikisha Waziri Mkuu
wa Ethiopia, pamoja na Marais wa Afrika Kusini, Mauritania, Gabon na
Senegal.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amepinga mpango huo, akisema huo ni uvamizi.
Uamuzi wake wa mwaka uliopita kutaka kugombea awamu ya tatu ulianzisha mapigano hayo ambapo kufikia sasa mamia ya watu wameuawa.
Viongozi wa Afrika waliokuwa wakikutana juma lililopita walighairi juu
ya swala la kuwatuma wanajeshi 5,000 wa kudumisha amani, na badala yake
wakaamua kutumia njia za kidiplomasia.